![]() |
| Tundu Lisu |
Tukio
la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antipas Lissu (Chadema) na
watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake jana mchana limeendelea kulaaniwa
vikali na watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa, viongozi wa dini na wananchi
mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii na media nyinginezo.
Lissu akiwa amefika nyumbani kwake Area D, eneo la Site Three, baada ya
kuahirishwa kwa kikao cha bunge, kabla hajashuka kwenye gari watu wasiojulikana
wakiwa kwenye gari linalodaiwa kuwa ni aina ya Nisani ambalo namba zake
hazikutambulika, walianza kumshambulia kwa risasi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Kamanda wa Polisi Dodoma, Gilles Muroto,
risasi
zilizotumika ni kati ya 28 mpaka risasi 32. Risasi kadhaa zilimpata
kwenye mwilini, mkononi risasi moja, miguuni risasi mbili na tumboni risasi
mbili, kwa hiyo jumla risasi tano zilimjeruhi. Baada ya tukio watu hao
walikimbia.
“Lissu alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa kutumia gari
la familia ya Naibu Spika kwa kuwa wanaishi jirani. Alipofikishwa aliingizwa
kwenye chumba cha upasuaji na kufanyiwa upasuaji kuzuia damu kuendelea kuvuja,
ambapo Katibu MKuu wa Wizara ya Afya aliongoza upasuaji huo kwa kushirikiana na
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
ulikuwa umeagiza ndege kwa ajili ya kumchukua mgonjwa kumpeleka Muhimbili.
Lakini familia na Mwenyekiti wa chadema Freeman Mbowe, walishauri apelekwe hospitali
ya Aga-Khan, Nairobi nchini Kenya kwa matibabu zaidi.
Aidha, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Vincent Mashinji amesema kuwa
amepokea taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman
Mbowe kuwa Tundu Lissu amezinduka leo asubuhi na kwa sasa anajitambua na
anaendelea vizuri.

No comments:
Post a Comment